UN yaiongezea MONUSCO muda wa kuhudumu nchini Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78308-un_yaiongezea_monusco_muda_wa_kuhudumu_nchini_kongo_dr
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeuongezea muda wa mwaka mmoja Ujumbe wake wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO na kuwataka walinda amani wa ujumbe huo kuelekeza nguvu zao Kaskazini-Mashariki mwa nchi, huku likisisitizia kufanyika operesheni za pamoja na vikosi vya nchi hiyo, FARDC.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 21, 2021 23:13 UTC
  • UN yaiongezea MONUSCO muda wa kuhudumu nchini Kongo DR

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeuongezea muda wa mwaka mmoja Ujumbe wake wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO na kuwataka walinda amani wa ujumbe huo kuelekeza nguvu zao Kaskazini-Mashariki mwa nchi, huku likisisitizia kufanyika operesheni za pamoja na vikosi vya nchi hiyo, FARDC.

Nchi zote 15 wanachama wa Baraza la Usalama zimepitisha azimio hilo la kurefusha muda wa kuhudumu walinda amani wa MONUSCO nchini Kongo DR.

Moja ya vipengee vya azimio hilo kinasema, hadi Desemba 20 mwaka 2022 Monusco itakuwa imehakikisha imebaki na wanajeshi 14,160 na maafisa wa polisi 2,001. 

Kwa mujibu wa azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, askari wa kulinda amani walioko mkoani Tanganyika kusini-mashariki mwa nchi, wataondolewa katikati ya mwaka wa 2022 na kuunganishwa na vikosi vya Umoja huo huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, majimbo matatu ambayo yanaendelea kushuhudia kuzorota kwa hali ya usalama kufuatia kuwepo kwa makundi yenye silaha.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Baraza la Usalama pia limesema kuna udharura wa kuheshimiwa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu; na limetilia mkazo pia kushirikishwa katika operesheni za pamoja vikosi vya jeshi la Kongo FARDC, ikiwa ni pamoja na brigedi yake ya kuingilia kati.

Azimio hilo limepitishwa wakati jeshi la Uganda limekuwa likifanya operesheni za pamoja za kijeshi na FARDC tangu Novemba 30 dhidi ya waasi wa ADF, ambao wamekuwa wakiua raia na kuchoma miji na vijiji ikiwemo magari, mashariki mwa nchi hiyo.

Majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri yamekuwa katika hali ya dharura na kuzingirwa tangu mwezi Mei, huku mauaji yakiendelea kuripotiwa.../