Tetesi za kuingia kwa mara nyingine NATO nchini Libya
Sambamba na kuongezeka matatizo ya kiusalama Libya, kuna taarifa kuwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO linapanga kuingilia tena kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, mnamo Jumatano 25 Mei akizungumza katika kikao cha pamoja na waandishi habari na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi, amesema kuwa, NATO iko tayari kuingilia kijeshi nchini Libya.
NATO ilikuwa kati ya wahusika wakuu wa mgogoro wa Libya ulioanza mwaka 2011. Shirika hili la kijeshi la nchi za Magharibi liliingia moja kwa moja kijeshi nchini Libya kwa msingi wa azimio nambari 1973 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuuawa dikteta wa miongo minne wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.
Kufuatia uingiliaji kijeshi huo wa madola ya Magharibi, Libya ilijipata katika mgogoro mpya wa kiusalama pamoja na kutoweka uthabiti wa kisiasa jambo ambalo liliitumbukza nchi hiyo katika vita vya ndani.
Mbali na mapigano baina ya mirengo na makundi mbali mbali ya kisiasa, sehemu kubwa ya Libya ilitekwa na kundi la kigaidi la Daesh au ISIS na makundi mengine ya wanamgambo.
Hivi sasa nchi hiyo ikiwa bado katika hali ya msukosuko na kukaliwa kwa mabavu baadhi ya maeneo yake na kundi la kigaidi la ISIS, kunasikika tetesi za uwezekano wa shirika la kijeshi la NATO kujiingiza tena nchini humo. Mara hii inaelekea NATO itajiingiza kwa njia tofautia Libya ikilinganishwa na mwaka 2011.
Duru za kidimplomasia zinadokeza kuwa, NATO inataka kuingia Libya kwa kisingizio cha kutoa mafunzo ya kijeshi kwa jeshi la nchi hiyo.
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya, tarehe 22 Mei alitangaza kuwa wakuu wa Libya wameomba rasmi msaada wa Umoja wa Ulaya katika kutoa mafunzo kwa polisi wa kulinda doria baharini na jeshi la wanamaji la nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, NATO hivi sasa haina uwezo wa kutumia mabavu na kuingia moja kwa moja kijeshi nchini Libya kama ilivyofanya mwaka 2011.
Katika upande mwingine hatupasi kusahau kuwa, kusambaratika na kudhoofika jeshi la Libya ni jambo ambalo lilichangia NATO kuingilia kijeshi nchini humo mwaka 2011.
Kwa vyovyote vile, iwapo NATO itajikita tu katika kutoa mafunzo kwa jeshi la Libya na serikali ya nchi hiyo nayo iunganishe makundi yote yenye silaha na kuunda jeshi la umoja wa kitaifa, basi Libya itaweza kufanikiwa katika vita vyake dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS.
Hivi sasa pia Jeshi la Libya linaendeleza mapigano makali na magaidi wa ISIS karibu na mji wa Benghazi. Viongozi wa Libya wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa hawataki vikosi vya kigeni nchini humo bali wanachohitaji ni msaada wa kimataifa wa silaha na mafunzo ya kijeshi ili kuweza kurejesha amani na utulivu nchini humo.