Upinzani Afrika Kusini wakituhumu chama tawala kuliteketeza kwa moto jengo la Bunge
(last modified Mon, 03 Jan 2022 12:18:14 GMT )
Jan 03, 2022 12:18 UTC
  • Upinzani Afrika Kusini wakituhumu chama tawala kuliteketeza kwa moto jengo la Bunge

Mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani nchini Afrika kusini amekituhumu chama tawala cha Kongresi ya Taifa cha nchi hiyo (ANC) kuwa kimehusika na moto ulioteketeza kikamilifu sehemu ya jengo la Bunge la nchi hiyo.

Shirika la habari la Sputnik limeripoti kuwa, mwaka 2017 tume iliundwa nchini Afrika Kusini kuchunguza madai ya ufisadi na ubadhirifu katika sekta ya umma. Tume hiyo iliwasilisha matokeo ya uchunguzi wake mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana kwa Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo na kulazimika kuweka wazi sehemu ya ripoti yake hiyo. 

Willie Madisha mbunge wa Afrika Kusini ambaye pia ni kiongozi wa zamani wa Muungano wa Walimu na ule wa Wafanyabiashara wa nchi hiyo ameashiria ripoti hiyo na kuongeza kuwa, anadhani taarifa zilizomo ndani ya ripoti hiyo zimetaja wazi ufisadi wa serikali ya Pretoria. Amesema, kwa mtazamo wake serikali inayoongozwa na Ramaphosa, mawaziri wake na shakhsia wengineo huwenda wamekusudia kuvuruga taarifa  ya uchunguzi wa tume hiyo. 

Willie Madisha 

Madisha ambaye alikuwa akizungumza bungeni amesema: "Nimestaajabishwa sana na moto huu hasa kwa kuizingatia kwamba jengo hili lilikuwa na ulinzi na usalama wa hali ya juu. Hata hivyo jambo la kuashiria hapa ni kwamba wakati wote panapojadiliwa masuala muhimu na nyeti kunakuwa na uwezekano wa kutokea jambo lolote la kusikitisha."

Moto ulitokea jana Jumapili katika eneo kongwe zaidi katika jengo la Bunge la Taifa la Afrika Kusini katika mji wa Cape Town; eneo ambalo lilikuwa likitumika kwa ajili ya vikao vya mabaraza ya kitaifa ya miji na pia vikao vya kamati mbalimbali. Moto huo ulitokea katika Bunge la Afrika Kusini masaa kadhaa baada ya kumbukumbu maalumu ya kumuenzi Askofu Desmond Tutu, mpigania ukombozi wa Afrika Kusini aliyefariki dunia hivi karibuni. 

Moto huo haujasababisha vifo wala majeruhi, na hadi sasa uchunguzi ungali unaendelea kubaini chanzo chake.