Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi yaendelea nchini Sudan
Wananchi wa Sudan wameendeleza maandamano yao ya kupinga utawala wa kijeshi na kwa mara nyingine wamewashinikiza wanajeshi warejee makambini na waruhusu raia waendeshe masuala ya kisiasa na kiutawala ya nchi hiyo.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, usiku wa kuamkia leo Ijumaa, maelfu ya Wasudan wanaopinga utawala wa kijeshi wameendeleza maandamano yao katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mingi ya Sudan. Wanajeshi na askari polisi wamejaribu kukandamiza maandamano hayo ingawa hawakufanikiwa kuyazima.
Kamati ya madaktari ya Sudan imesema kuwa, raia mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la nchi hiyo huku waandamanaji wengine wengi wakijeruhiwa katika maandamano hayo ya jana usiku.
Maandamano hayo yamepamba moto baada ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kutangaza kujiuzulu Jumapili usiku. Utawala wa majenerali wa kijeshi nchini Sudan umemimina askari wake katika kila kona, lakini pamoja na hayo maandamano yanaendelea.
Mara zote askari wa Sudan wanawashambulia waandamanaji katika maeneo tofauti ya nchi hiyo lakini kadiri ukandamizaji wa askari huo unavyoongezeka, ndivyo wananchi wa nchi hiyo wanavyozidi kupanda mori na hamasa ya kuendeleza maandamano yao hadi wawalazimishe wanajeshi warejee makambini.
Wimbi la hivi sasa la maandamano lilizuka tarehe 25 Oktoba 2021 baada ya majenerali wa kijeshi kufanya mapinduzi mengine yaliyoipindua serikali ya mpito ambayo ndani yake ilikuwa imeshirikisha pia viongozi wa kiraia. Kabla ya hapo pia jeshi la Sudan lilitumia vibaya maandamano ya wananchi, likafanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Jeneral Omar al Bashir na baadaye jeshi hilo kung'ang'ania madaraka hadi leo hii.