Wanavijiji 200 wameuawa katika mashambulizi ya Zamfara Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79006-wanavijiji_200_wameuawa_katika_mashambulizi_ya_zamfara_nigeria
Viongozi wa serikali katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria wametangaza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia katika mashambulizi ya magenge ya wabeba silaha katika eneo hilo imeongezeka na kufikia watu 200.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2022 10:04 UTC
  • Wanavijiji 200 wameuawa katika mashambulizi ya Zamfara Nigeria

Viongozi wa serikali katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria wametangaza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia katika mashambulizi ya magenge ya wabeba silaha katika eneo hilo imeongezeka na kufikia watu 200.

Balarabe Alhaji, kiongozi wa kijamii amesema wameshazika watu 143 waliouawa katika mashambulizi hayo katika vijiji kadhaa vya jimbo la Zamfara.

Mmoja wa wakazi wa vijiji vilivyoshambuliwa, Ummaru Makeri, ambaye amepoteza mkewe na watoto katika hujuma hizo, amesema idadi ya waliouawa katika kipindi cha wiki moja iliyopita ni watu zaidi ya 150.

Hata hivyo wiongozi na wanavijiji wa jimbo hilo wamethibitisha kupatikana miili ya watu 200, huku wakitahadharisha juu ya uwezekano wa kupatikana miili mingi zaidi.

Magenge ya wabeba silaha jimboni Zamfara

Hii ni katika hali ambayo, maafisa wa polisi walisema hivi karibuni kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika hujuma hizo, walikuwa 58 pekee.

Maafisa usalama wamesema wamefanikiwa kuangamiza wabeba silaha 100 katika mashambulizi ya anga dhidi ya maficho ya wavamizi hao.

Licha ya kwamba jeshi la Nigeria lilipiga kambi katika jimbo hilo mwaka 2016 kwa ajili ya kuimarisha usalama, lakini bado makundi ya wabeba silaha ambayo yamekuwa yakifanya wizi na magendo, yanaendelea kufanya jinai na uhalifu.