Wanafunzi 30 waliotekwa nyara waachiwa huru kaskazini magharibi mwa Nigeria
Wanafunzi waliokuwa wametekwa nyara kaskazini magharibi mwa Nigeria wameachiwa huru baada ya kushikiliwa na wanamgambo wenye silaha kwa muda wa miezi saba.
Wanafunzi hao walitekwa nyara na wanamgambo wenye silaha karibu miezi saba iliyopita katika jimbo la Kebbi huko Nigeria. Maafisa wa serikali ya Nigeria wameeleza kuwa, wanafunzi hao waliwasili katika makao makuu ya jimbo hilo huko Kevi wakiwa pamoja na mwalimu wao. Msemaji wa Gavana wa Kevi ameeleza kuwa, suala la kutoa hongo kwa makundi ya wahalifu wenye silaha ili wawaachie huru mateka limekuwa jambo la kawaida.
Kitengo Kinachohusika na Masuala ya Watoto cha Umoja wa Mataifa kimeripoti kuwa, hadi sasa zaidi ya watoto 1,400 wametekwa nyara nchini Nigeria. Wakati huo huo wakazi wa jimbo la Kebbi wameeleza kuwa, hadi sasa hawajajua ni watu wangapi wametoweka tangu kujiri shambulio katika shule ya Kebi na kutekwa nyara wanafunzi.
Hili ni kundi la tatu la wanafunzi kuachiwa huru jimboni humo tangu baada ya tukio hilo la utekaji nyara miezi saba iliyopita. Kundi jingine la wanafunzi waliokuwa wametekwa nyara liliachiwa huru mwezi Oktoba mwaka jana. Maafisa wa serikali za mitaa na wanafunzi wanaoachiwa huru wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mara nyingi wanafunzi wanaachiwa huru kwa awamu na si kwa mkupuo kwa kuzingatia kuwa kila awamu ya kuachiwa huru inakwenda sambamba na fedha za kikomboleo.