Waislamu Afrika Kusini wataka kulindwa turathi za kale Cape Town
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79260-waislamu_afrika_kusini_wataka_kulindwa_turathi_za_kale_cape_town
Wanaharakati wa Kiislamu katika wilaya ya Bo-Kaap jijini Cape Town nchini Afrika Kusini wametoa mwito wa kulindwa na kuhifadhiwa turathi na athari za kale hususan za kidini katika eneo hilo ambalo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 16, 2022 08:05 UTC
  • Waislamu Afrika Kusini wataka kulindwa turathi za kale Cape Town

Wanaharakati wa Kiislamu katika wilaya ya Bo-Kaap jijini Cape Town nchini Afrika Kusini wametoa mwito wa kulindwa na kuhifadhiwa turathi na athari za kale hususan za kidini katika eneo hilo ambalo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu.

Mwanaharakati na wakili maarufu katika eneo hilo, Seehaam Samaai ameliambia shirika la habari la Anadolu la Uturuki kuwa, kubadilishwa utambulisho wa wilaya hiyo na mabwenyenye ni moja ya changamoto kuu zinazolikabili eneo hilo la Waislamu katika kipindi hiki cha baada ya enzi za mfumo wa kibaguzi (apartheid).

Amesema matajiri wamevamia wilaya ya Bo-Kaap na kujenga majengo mapya ya kisasa, huku yale ya kale yakitoweka siku baada ya siku, huku turathi za kihistoria, kitamaduni na kidini za eneo hilo zikifutika taratibu.

Mwanaharakati huyo amevitaka vyombo husika vya serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka na za makusudi kulilinda eneo hilo na turathi zake za kihisoria zinazoelekea kutoweka.

Seehaam Samaai amesisitiza kuwa, "Kuna haja ya kuijumuisha Bo-Kaap katika orodha ya maeneo yenye turathi za kale yanayolindwa na sheria iliyopasishwa mwaka 2019."

Msikiti Afrika Kusini

Amesema iwapo Bo-Kaap ambayo akthari ya wakazi wake ni Waislamu itawekwa kwenye orodha hiyo, basi wajasiriamali wanaotaka kwenda katika eneo hilo watatakiwa kuzingatia na kuheshimu turathi za kale za wilaya hiyo.

Mkereketwa na mtaalamu huyo wa sheria wa Afrika Kusini amesema eneo hilo lilijengwa na Waislamu ambao asili yao ni Malaysia, waliopelekwa Afrika Kusini kama watumwa na wakoloni wa Uholanzi miaka ya 1790, lakini hivi sasa wakazi wake wamelazimika kuhamia maeneo mengine ya Cape Town baada ya kufurushwa na mabwanyenye, ambao wanaharibu athari za kale za eneo hilo.