Madaktari Sudan waandamana kulaani ukandamizaji wanaotendewa na jeshi
Madaktari nchini Sudan wameshiriki katika maandamano kulaani vikali ukandamizaji na mabavu yanayotumiwa dhidi ya madaktari na wauguzi wanatoa huduma wakati wa maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Maandamano hayo ya Jumapili ni katika mfululizo wa maandamano ambayo yanafanyika karibu kila siku Sudan huku jeshi likiendelea kutumia mabavu kukandamiza maandamano hayo ya amani.
Mmoja wa madaktari aliyeshiriki katika maandaman hayo mjini Khartoum amesema katika kila maandamano, wanajeshi hurusha gesi ya kutoa machozi karibu na hospitali. Amesema hata baadhi ya askari hushambulia chumba cha wagonjwa mahututi.
Hali inazidi kuwa mbaya nchini Sudan, ambapo nchi imeathiriwa na ghasia na mapigano kati ya askari usalama na waandamanaji wanaopinga mapinduzi ya wanajeshi yaliyojiri nchini humo Oktoba 25 mwaka jana.
Licha ya wanajeshi huko Sudan kuahidi kuwa watakabidhi mamlaka ya uongozi kwa raia lakini wale wanaopinga utawala wa kijeshi nchini humo wanalitaka jeshi kuondoka madarakani na kuundwa serikali halali na ya kidemokrasia nchini humo.
Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa tangu jeshi la Sudan litwae madaraka ya nchi Oktoba 25 mwaka jana imepindukia 55.
Hivi karibuni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilitangaza kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada zake za kupatanisha makundi yote ya kisiasa Sudan ili kutatua mgogoro unaoendelea kutokota nchini humo.
Mpango mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutatua mgogoro wa Sudan una vipengee vinne ambapo kipengee muhimu zaidi ni kuvunjwa Baraza la Utawala na nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Uongozi litakaloundwa na watu watatu wasio wanajeshi.