Maambukizi ya aina mpya ya spishi ya Omicron yachachamaa Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79988-maambukizi_ya_aina_mpya_ya_spishi_ya_omicron_yachachamaa_afrika_kusini
Afrika Kusini imeshuhudia ongezeko la maambukizi ya aina mpya ya spishi ya kirusi cha Corona cha Omicron, iliyopewa jina la kitaalamu la BA.2.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2022 01:08 UTC
  • Maambukizi ya aina mpya ya spishi ya Omicron yachachamaa Afrika Kusini

Afrika Kusini imeshuhudia ongezeko la maambukizi ya aina mpya ya spishi ya kirusi cha Corona cha Omicron, iliyopewa jina la kitaalamu la BA.2.

Wanasayansi wa Afrika Kusini wamesema kasi ya maambukizi ya Corona nchini humo inatokana na maambukizi ya spishi hiyo mpya BA.2 ambayo inaenea kwa kasi zaidi ya kirusi cha asili cha Omicron.

Michelle Groome, mwanasayansi mwandamizi wa Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukizwa nchini Afrika Kusini amesema, asilimia 23 ya sampuli 450 zilizofanyiwa uchunguzi mwezi uliopita wa Januari, inajumuisha kesi za aina hiyo mpya ya Corona.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), aina hiyo mpya ya spishi ya kirusi cha Corona cha Omicron imeripotiwa katika nchi 57 duniani kufikia sasa zikiwemo tano za Afrika, ambazo ni Afrika Kusini, Kenya, Botswana, Malawi na Senegal.

Hata hivyo akthari ya kesi za maambukizi ya aina mpya ya Omicron zimeripotiwa katika nchi za Ulaya, Asia na Marekani. Kwa wastani, Wamarekani 2,500 wanaaga dunia kila siku hivi sasa kutokana na maradhi ya Covid-19.

Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwisho wa mwezi Desemba 2019 lilipoibuka janga la Corona hadi sasa, zaidi ya watu 241,000 wameaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 barani Afrika, huku watu milioni 11 wakiambukizwa maradhi hayo katika nchi za bara hilo.