Maandamano mapya ya Wasudan ya kupinga utawala wa kijeshi
Mamia ya wananchi wa Sudan jana Jumatatu kwa mara nyingine tena waliandamana katika mji mkuu Khartoum kupinga utawala wa kijeshi nchini humo.
Maandamano ya jana yaliitishwa na wanachama wa Kamati ya Mapambano na Chama cha Wanataaluma Sudan (SPA) waliiongoza maandamano yaliyomng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.
Mmoja wa waandamanaji hao katika eneo la Bashdar jijini Khartoum, Emad Alhassan amesema wataedeleza maandamano hayo licha ya kushambuliwa na kuuawa na maafisa usalama.
Takwimu za madaktari zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu 80 wamethibitishwa kuuawa na mamia ya wengine wameshajeruhiwa katika maandamano hayo ambayo yalianza Oktoba wakati Jeshi lilipotangaza kutwaa madaraka kikamilifu nchini humo.
Wiki iliyopita pia, waandamanaji nchini Sudan waliendelea na maandamano yao kwa kufunga barabara kuu inayounganisha mpaka wa Sudan na Misri ikiwa ni katika jitihada zao za kuwalazimisha majenerali wa kijeshi wang'oke madarakani. Wanaituhumu Cairo kuwa inawaunga mkono majenerali wa kijeshi waliotwaa madaraka ya nchi.
Maandamano ya nchini Sudan yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi mengine mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021 ambayo yaliiondoa madarakani serikali iliyokuwa inashirikisha pia raia nchini humo.