Wasudan waandamana kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel
(last modified Fri, 11 Feb 2022 10:39:00 GMT )
Feb 11, 2022 10:39 UTC
  • Wasudan waandamana kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel

Wananchi wa Sudan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa majenerali wa kijeshi nchini mwao.

Mwezi Oktoba 2021, wanajeshi wa Sudan walifanya mapinduzi mengine wakiongozwa na Jenerali Abdul Fattah al Burhan na waliipindua serikali ya Waziri Mkuu Abdullah Hamdok ambayo ilikuwa inashirikisha pia raia. 

Maandamano ya wananchi yalipamba moto baada ya mapinduzi hayo kiasi kwamba, tarehe 21 Novemba mwaka huo huo wa 2021 majenerali wa kijeshi nchini Sudan walilazimika kumrejesha madarakani Hamdok ambaye alisema amekubali kurudi madarakani ili kuzuia kuendelea kumwagika damu za wananchi na kwa sharti kwamba, majenerali hao waheshimu Katiba.

Wanajeshi Sudan wamewekwa vizuizi vingi lakini maandamano ya wananchi bado yanaendelea

 

Hata hivyo kurejea madarakani Hamdok hakukuzuia wala kupunguza maandamano ya wananchi wala ukandamizaji wa wanajeshi. Hivyo Abdulla Hamdok aliamua kujiuzulu nafasi yake ya Waziri Mkuu na hadi hivi sasa maandamano yanaendelea ili kuwalazimisha majenerali wa kijeshi nchini Sudan warudi katika kambi zao na waruhusu wananchi waendeshe serikali kikatiba.

Maandamano ya wananchi wa Sudan yaliendelea tena jana Alkhamisi na mara hii, mbali na kushinikiza majenerali wa kijeshi warejee makambini, wameulaani utawala wa Kizayuni wa Israel wakisema kuwa, Sudan kamwe haiwezi kuutambua rasmi utawala katili wa Israel.

Waandamanaji walibeba mabango ambayo baadhi yake yalikuwa yameandikwa maneno yafuatayo: "Abdul Fattah al Burhan, kibaraka wa utawala wa Kizayuni; ataanguka tu."

Juzi Jumatano, shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa, mwakilishi mmoja wa serikali ya kijeshi ya Sudan ametembelea Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa ziara rasmi ya kikazi.

Tags