Karibu watoto milioni tatu kupata chanjo ya polio Malawi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81026-karibu_watoto_milioni_tatu_kupata_chanjo_ya_polio_malawi
Madaktari na wauguzi watatoa chanjo za kujikinga na ugonjwa wa polio kwa watoto wasiopungua milioni 2.9 huko Malawi. Hayo yameelezwa na Umoja wa Mataifa baada ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu kuugua ugonjwa huo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 04, 2022 23:23 UTC
  • Karibu watoto milioni tatu kupata chanjo ya polio Malawi

Madaktari na wauguzi watatoa chanjo za kujikinga na ugonjwa wa polio kwa watoto wasiopungua milioni 2.9 huko Malawi. Hayo yameelezwa na Umoja wa Mataifa baada ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu kuugua ugonjwa huo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.

Hiyo ni kesi ya kwanza ya maambukizi ya kirusi cha polio mwitu kuwahi kuripotiwa huko Malawi kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Nchi hiyo ya kusini mwa bara la Afrika wiki mbili zilizopita ilitangaza kuathiriwa na mlipuko wa polio baada ya sampuli zilizopelekwa maabara kuthibitisha uwepo wa maambukizi na kuonyesha aina ya kirusi hicho kuwa na mahusiano na kile kilichoenea sasa huko Pakistan.  

Rudolf Schwenk Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa nchini Malawi (UNICEF) amesema kuwa, kuibuka tena kwa virusi vya polio mwitu nchini Malawi ni jambo lenye kutia wasiwasi mkubwa.

Athari za kutopata chanjo ya polio 

Amesema utoaji chanjo ni njia pekee ambayo itawalinda watoto wa Malawi na ugonjwa huo unaoambukiza sana na ambao unasababisha ulemavu.

Infaaa kuashiria hapa kuwa, Polio ni ni miongoni mwa magonjwa mabaya ya kuambukiza ambao hushambulia mfumo wa neva na unaweza kusababisha kupooza kabisa viungo vya mwili ndani ya masaa machache. 

Hadi hivi sasa ugonjwa huo ukiwa hauna tiba lakini unaweza kuzuiwa kwa kutolewa chanjo kwa watoto.

Shirika la Unicef nchini Malawi limesema kuwa, litanunua na kusambaza dozi milioni 6.9 za chanjo ya polio kwa watoto wote walio na  umri wa chini ya miaka mitano.