Afrika Kusini yataka Afrika itumie sarafu moja itakayoimarisha biashara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81258-afrika_kusini_yataka_afrika_itumie_sarafu_moja_itakayoimarisha_biashara
Afrika Kusini imesema inaunga mkono wazo la kuanzisha sarafu moja ambayo itapiga jeki miamala ya kibiashara miongoni mwa nchi za bara hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2022 04:41 UTC
  • Afrika Kusini yataka Afrika itumie sarafu moja itakayoimarisha biashara

Afrika Kusini imesema inaunga mkono wazo la kuanzisha sarafu moja ambayo itapiga jeki miamala ya kibiashara miongoni mwa nchi za bara hilo.

Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini amesema kama nchi hiyo ilivyofanywa katika majukwaa na mikutano mbalimbali ya Afrika, itaendelea kuunga mkono Mkataba wa Abuja wa mwaka 1991, unaotaka nchi za bara Afrika zitangamane na ziondokane na vizingiti na vikwazo vya kibiashara.

Pandor amesisitiza kuwa, "Kuundwa Benki Kuu ya Afrika (ACB), Benki ya Uwekezaji Afrika (AIB) na Shirika la Fedha la Afrika (AMI) ni suala muhimu ambalo litafanikisha mchakato wa kuanzisha sarafu moja ya Afrika, itakayoimarisha biashara miongoni mwa nchi za bara hili."

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini ameongeza kuwa, kuzinduliwa rasmi Eneo la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA) mnamo Januari Mosi 2021, ilikuwa hatua kubwa katika kujumuisha soko la pamoja la nchi za Afrika. Mpango huo unatazamiwa kuongeza biashara kati ya mataifa ya Afrika kutoka 18% hadi 50% ifikapo mwaka 2030.

Shehena za mizigo

Mwaka jana Jumuiya ya Uchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS ilipasisha ramani mpya ya njia ya uzinduzi wa sarafu moja mwaka 2027, baada ya mpango wa awali wa kuzindua sarafu hiyo kuvurugwa na janga la Corona.

Nchi wanachama wa ECOWAS zinatarajia kuwa, matumizi ya sarafu hiyo iliyopewa jina la 'Eco' yatapiga jeki biashara na ustawi wa chumi za nchi hizo za Magharibi mwa Afrika.