WFP yatahadharisha kuhusu hatari ya njaa nchini Sudan Kusini
Katika taarifa yake mpya, Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetahadharisha kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Sudan Kusini mwaka huu wa 2022 wanakabiliwa na hatari ya njaa.
Miaka 10 baada ya kujitenga na Sudan na kuwa huru, Sudan Kusini imeendelea kuwa moja ya nchi maskini duniani ambapo asilimia 82 ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini licha ya maliasili ya mafuta iliyonayo na misaada mbalimbali ya kimataifa inayopokea.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wenye mfungamano na Umoja wa Mataifa umetangaza leo Jumamosi kuwa, baa la njaa linatazamiwa kuwaathiri mamilioni ya watu huko Sudan Kusini; ambao wanataabika na maafa na taathira za mafuriko na kuibuka tena mapigano ya ndani.
Shirika la WFP limeongeza kuwa, mgogoro wa njaa unainyemelea Sudan Kusini wakati huu ambapo taasisi za kimataifa zimejkita katika mgogoro wa Ukraine. Kwa mujibu wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) makumi ya maelfu ya watu huko Sudan Kusini wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na majanga ya kimaumbile na machafuko.
WFP aidha limetahadharisha kuwa, karibu watu milioni 8.3 wa Sudan Kusini, wakiwemo wakimbizi, wanakaribia kupatwa na njaa katika miezi ijayo. Adeyinka Badejo Naibu Mkurugenzi wa shirika la WFP nchini Sudan Kusini amesema kuwa kiwango cha hali hiyo ya njaa kinatia wasiwasi.