Jeshi la Sudan: Tutakabidhi madaraka kwa serikali itakayochaguliwa
Naibu kiongozi wa baraza la uongozi la Sudan amesisitiza kuwa, utawala wa mpito wa kijeshi nchini humo utakabidhi madaraka kwa serikali itakayochaguliwa.
Mohamed Hamdan Dagalo alisema hayo jana Jumamosi akinukuu taarifa ya baraza kuu la uongozi la Sudan na kueleza kuwa, "Tumejitolea kukabidhi madaraka kwa wazalendo (wenzetu) baada ya kupatikana mwafaka wa kitaifa utakaopelekea kufanyika uchaguzi."
Ameeleza bayana kuwa, wanajeshi wanaoongoza hivi sasa Sudan watarejea makambini, baada ya kuja serikali itakayochaguliwa na wananchi kupitia masanduku ya kupigia kura.
Hata hivyo naibu kiongozi huyo wa baraza la uongozi la Sudan amesisitiza kuwa, utawala wa kijeshi hautakabidhi madaraka kwa baadhi ya wanasiasa ambao wapo katika 'orodha ya mishahara' ya balozi kadhaa za maajinabi nchini humo.
Kwa miezi kadhaa sasa, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo kupinga utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao wamekuwa wakishinikiza kurejeshwa serikali ya kiraia nchini Sudan sambamba na kupinga utawala wa kijeshi tokea Oktoba 25 mwaka jana.