Watu 16 wauawa katika shambulizi la 'magaidi' Zamfara Nigeria
Kwa akali watu 16 wameuawa katika shambulizi la genge la wabeba silaha katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Mohammed Shehu, Msemaji wa Polisi katika jimbo la Zamfara amesema wavamizi hao wameshambulia kijiji cha Ganar-Kiyawa katika wilaya ya Bukkuyum, na kuua wanakijiji 16 kwa kuwapiga risasi.
Amesema maafisa usalama wanafanya msako mkali wa kuzuia mashambulizi zaidi na kuwasaka wahalifu hao aliowataja kuwa magaidi.
Hata hivyo vyombo vya habari katika eneo hilo vimesema idadi ya wanakijiji waliouawa katika shambulio hilo jipya la magenge ya wabeba silaha jimboni Zamfara ni watu 37, akiwemo chifu wa kijiji hicho.
Licha ya kwamba jeshi la Nigeria lilipiga kambi katika jimbo hilo mwaka 2016 kwa ajili ya kuimarisha usalama, lakini bado makundi ya wabeba silaha ambayo yamekuwa yakifanya wizi na magendo, yanaendelea kufanya jinai na uhalifu.
Mapema mwaka huu, wanavijiji 200 waliuawa katika mashambulizi mengine ya makundi hayo ya wabeba silaha katika jimbo hilo la Zamfara la kaskazini magharibi mwa Nigeria.