Wasudan waandamana usiku kucha dhidi ya serikali ya kijeshi
Wananchi wa Sudan wameendelea kuandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na katika miji mingine ya nchi hiyo dhidi ya serikali ya kijeshi.
Maandamano na machafuko makubwa yameigubika Sudan katika miezi ya karibuni kufuatia jeshi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Wafanya maandamano wanataka wanajeshi waondoke madarakani, uongozi wa nchi ukabidhiwe raia, uchaguzi wa kidemokrasia uitishwe nchini humo sambamba na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi nchini.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, viongozi wa jeshi na wa kiraia huko Sudan wamekuwa wakipingana tangu mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir kupinduliwa miaka miwili iliyopita na serikali ya mpito kuanzishwa.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, maelfu ya wananchi wa Sudan jana waliandamana usiku katika mitaa ya mji mkuu Khartom na mbele ya jengo la bunge la taifa katika mji wa Umdurman magharibi mwa Khartoum. Askari usalama walifika mbele ya bunge na kuanza kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi na kufyatulia risasi ili kuwatawanya waaandamanaji waliokuwa wamekusanya hapo.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mtu mmoja ameuawa katika ghasia huko Khartoum. Umoja wa Mataifa pia umeeeza kutiwa wasiwasi na kuongezeka ghasia huko Sudan na kutahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya binadamu na njaa nchini humo.