Watu wanne waaga dunia baada ya boti yao kuzama pwani ya Libya
Kwa akali watu wanne wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika Bahari ya Mediterrania, pwani ya Libya.
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, boti hiyo hafifu iliondoka mji wa Surman, kaskazini magharibi mwa Libya siku ya Jumapili, ikiwa imebeba wahajiri 20, kabla ya kuzama jana Jumatatu.
Taarifa ya IOM iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter imebainisha kuwa, miili minne imeopolewa baharini kufikia sasa, watu wawili wamenusuriwa, huku wengine 14 wakitoweka.
Haya yanajiri chini ya saa 48 baada ya wahajiri 13 wakiwemo watoto sita kufa maji baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Tunisia, wakijaribu kuelekea Italia.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM), tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, watu 475 wamekufa maji wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya kinyume cha sheria.
Wahajiri karibu 3,000 walikufa maji baharini wakati wakijaribu kuelekea barani Ulaya kwa kutumia maeneo ya kaskazini mwa Afrika mwaka jana 2021.