Chanjo ya Malaria imewafikia zaidi ya watoto milioni moja barani Afrika
Watoto zaidi ya milioni moja huko Ghana, Kenya na Malawi tayari wamepata dozi ya chanjo ya kwanza ya kujilinda na ugonjwa wa malaria isiyopungua moja.
Taarifa zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani zimeeleza kuwa, mpango wa majaribio uliozinduliwa Aprili 2019 ulikuwa salama na ulipunguza kwa kiasi kikubwa kesi kali za ugonjwa huo. Chanjo hiyo ya Malaria kwa jina la RTS,S inaweza kuokoa maisha ya watoto 40,000 hadi 80,000 kwa mwaka katika chini zilizo chini ya Jangwa la Sahara na katika maeneo yenye hatari kubwa.
Chanjo mpya ya Malaria inafanya kazi dhidi ya kijidudu maradhi kwa jina la Plasmodium Falcipalum ambacho ni hatari zaidi duniani na kinashuhudiwa zaidi katika nchi za Afrika. Karibu asilimia 90 ya kesi za ugonjwa wa Malaria zipo barani Afrika; ambapo watoto 260,000 huaga dunia kila mwaka kwa ugonjwa huo. Kimelea kinachosababisha ugonjwa wa Malaria hubebwa na mbu wa jamii ya kike aina ya Anopheles.
Malaria ni ugonjwa mkongwe sana na unaweza kuhatarisha maisha iwapo mgonjwa hatapata matibabu kwa haraka. Aidha zaidi ya dola milioni 155 zimekusanywa na Muungano wa Chanjo (GAVI) kwa lengo la kuwezesha usambazaji wa chanjo za Malaria. Siku ya kimataifa ya Malaria huadhimishwa kila mwaka duniani ifikapo tarehe 25 mwezi Aprili.