Polisi washambulia waandamanaji nchini Sudan
(last modified Sun, 01 May 2022 08:17:18 GMT )
May 01, 2022 08:17 UTC
  • Polisi washambulia waandamanaji nchini Sudan

Polisi nchini Sudan wamewashambulia waandamanaji ambao walikuwa wamekusanyika katika mji mkuu, Khartoum na miji mingine wakipinga utawala wa kijeshi sambamba na kuadhimisha mwaka wa tatu wa mauaji ya waandamanaji.

Mjini Khartoum jana Jumamosi waandamanaji walifunga barabara na kuanza kujitayarisha kufungua saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Hata hivyo kabla ya Magharibi maafisa wa polisi walivamia mjumuiko huo kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na kuwatawanya waandamanaji hao.

Maandamano pia yameripotiwa katika miji mingine mikubwa kama vile Madani, Kosti, El Obeid huku waandamanaji wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na picha za baadhi ya vijana waliouawa mwaka 2019.

Duru huru zinasema, hadi sasa watu zaidi ya 130 wameuawa Sudan katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini humo.

Maandamano Sudan

Kwa muda wa zaidi ya miaka miwili sasa maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika nchini Sudan kupinga utawala wa kijeshi na kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi. Omar al Bashir aliyetawala Sudan kwa muda wa miaka 30 alipinduliwa Aprili 2019 na Agosti mwaka huo huo utawala wa mpito wa jeshi na raia uliteuliwa kuongeza nchi. Hata hivyo mkuu wa majeshi ya Sudan, Abdel Fattah al Burhan ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa rais, alipindua serikali Oktoba mwaka jana na kuwatimua raia serikalini. Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ambaye alikuwa anaongoza mrengo wa raia katika serikali ya Sudan alikamatwa na kisha kuachiliwa huru.

Mapinduzi hayo yaliibua maandamano makubwa na yalilaaniwa kimataifa. Sudan, yenye idadi ya watu milioni 45 inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambapo mfumuko wa bei sasa umefika asilimia 400.

Tags