Rais wa AfDB atahadharisha: Janga la uhaba mkubwa wa chakula linainyemelea Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i84374-rais_wa_afdb_atahadharisha_janga_la_uhaba_mkubwa_wa_chakula_linainyemelea_afrika
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) amesema, vita kati ya Russia na Ukraine vitasababisha matatizo mengi katika kudhamini chakula kwa ajili ya wakazi wa bara hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2022 07:12 UTC
  • Rais wa AfDB atahadharisha: Janga la uhaba mkubwa wa chakula linainyemelea Afrika

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) amesema, vita kati ya Russia na Ukraine vitasababisha matatizo mengi katika kudhamini chakula kwa ajili ya wakazi wa bara hilo.

Akinwumi Adesina ametahadharisha kuwa, kutokana na uhaba unaozikabili taasisi kuu za kilimo, hali hiyo mbaya inaweza kupelekea chakula kupungua kwa asilimia 20 hadi 50 kwa mwaka barani Afrika.

Adesina ameongezea kwa kusema: "bara hili linaagiza kila mwaka karibu tani milioni mbili za mbolea kutoka Russia na Ukraine. Kwa hivyo ni wazi kuwa tunakabiliwa na hali mbaya sana tarajiwa ya uhaba wa chakula."

Rais wa AfDB ambaye amezungumza hayo leo wakati akiendelea na ziara yake ya siku nne nchini Kenya amebainisha kwamba, changamoto za hakikisho la upatikanaji wa chakula katika bara la Afrika zitaongezeka kwa sababu uingizaji wa mazao ya kilimo pia utaathiriwa.

Akinwumi Adesina

Dakta Akinwumi Adesina amefichua kuwa bara la Afrika litakosa takriban tani milioni 30 za mahindi, ngano na soya ambazo huwa linaagiza kila mwaka kutoka Russia na Ukraine. Ameendelea kueleza kwamba, mgogoro wa vita vya Russia na Ukraine umekuwa na taathira hasi pia kwa bei ya nishati katika bara la Afrika, hali ambayo itapelekea kupungua ukuaji wa uchumi pia katika bara hilo.

Hivi karibuni, Benki ya Maendeleo Afrika ilitenga dola bilioni 1.5 kusaidia kupunguza hali mbaya ya uhaba wa chakula katika nchi za bara hilo.

Dakta Akinwumi Adesina alitoa indhari pia hivi karibuni kwamba uzalishaji wa chakula barani Afrika utapungua kwa asilimia 20 na bara hilo litakosa mazao ya kilimo yenye thamani ya dola bilioni 11.

Kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa kupanda sana kwa bei za vyakula na nishati kutokana na vita vya Ukraine kunaliweka bara la Afrika kwenye hatari ya kukumbwa na hali mbaya ambayo haijawahi kushuhudiwa.../