Makundi ya kisiasa Sudan yabeza kuondolewa sheria ya hali ya hatari
(last modified Sat, 04 Jun 2022 12:48:42 GMT )
Jun 04, 2022 12:48 UTC
  • Makundi ya kisiasa Sudan yabeza kuondolewa sheria ya hali ya hatari

Makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan likiwemo la muungano wa vyama vya wafanyakazi yamesema, kufutwa sheria ya hali ya hatari nchini humo hakuna faida yoyote kwa sababu ukatili na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama ungali unaendelea.

Makundi hayo yamesisitiza kuwa yanapinga kuwa na maelewano na kufanya mapatano ya aina yoyote ile na wanajeshi wanaotawala na yanaitakidi kuwa, uamuzi huo wa kufutwa sheria ya hali ya hatari hauna faida yoyote kwa sababu vyombo vya usalama vingali vinaendelea kuwatia nguvuni waandamanaji kinyume cha sheria.

Muhand Mustafa, msemaji wa muungano wa wafanyakazi nchini Sudan ameeleza kwamba, wafanyamapinduzi ya kijeshi wamechukua uamuzi wa kuondoa sheria ya hali ya hatari kwa sababu walipotekeleza sheria hiyo walidhani kimakosa kwamba wataweza kuzima harakati za wapinzani, lakini kilichojiri ni kinyume na hivyo, kwa sababu maandamano ya upinzani yalipamba moto zaidi na wananchi hawakuipa umuhimu wowote sheria hiyo ya hali ya hatari.

Jenerali Abdel Fattah el Burhan

Jenerali Abdel Fattah el Burhan, mkuu wa baraza la utawala la Sudan hivi karibuni alitoa amri ya kuondolewa sheria ya hali ya hatari nchini humo na kuachiwa huru watu waliowekwa kizuizini.

Sheria ya hali ya hatari ilitangazwa nchini Sudan tangu jeshi lilipofanya mapinduzi Oktoba 25, 2021.../

Tags