Boko Haram yadhibiti mji wa mpaka na Niger
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la Nigeria limeteka na kudhibiti mji wa Bosso, ulioko kusini mashariki mwa mpaka wa Niger.
Habari zinasema kuwa, magaidi hao waliteka mji huo jana Ijumaa baada ya kujiri makabiliano makali kati yao na jeshi la Niger katika mji huo, yapata kilomita 1365 kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey. Mapigano hayo yamesababisha wanajeshi wa Niger kulikimbia eneo hilo na hivyo kutoa mwanya wa magaidi hao kulidhibiti. Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi hao waliingia katika mji huo kwa kutumia mto Komadougou Yobe, ulioko katika mpaka wa nchi mbili hizo za magharibi mwa Afrika.
Siku chache zilizopita, Jeshi la Niger lilitangaza kuwa limeangamiza wanachama 12 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika kijiji cha Bosso, kusini mashariki mwa eneo la Diffa karibu na mpaka na Nigeria.
Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Kundi hilo pia limepanua mashambulizi yake ya kigaidi katika nchi jirani kama Cameroon, Chad na Niger. Licha ya nchi kadhaa za Kiafrika kuungana kwa ajili ya kupambana na kundi la Boko Haram, lakini hadi sasa zimeshindwa kuwatokomeza wanamgambo hao.