Watu wasiopungua 27 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan
Watu wasiopungua 27 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika mapigano yaliyotokea kwenye maeneo ya magharibi na kusini ya Sudan.
Mashuhuda wamesema, katika matukio tofauti, mapigano yamezuka kwenye eneo tete kiusalama la Darfur yaliyochochewa na ugomvi mkubwa wa kugombea ardhi na kusababisha watu 16 kuuawa.
Watu wengine 11 wameuawa katika jimbo la Kordofan Kusini baada ya ugomvi baina ya watu wawili kupamba moto na kuishia kwenye mapigano ya kufyatuliana risasi.
Machafuko hayo yanaripotiwa huku Sudan ikiwa imegubikwa na wimbi la machafuko yaliyosababishwa na mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka uliopita yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Ripoti zinasema, katika jimbo la Darfur Magharibi linalopakana na Chad, mapigano yalizuka karibu na Kolbus, eneo lililoko umbali wa kilomita 160 kutoka El Geneina, makao makuu ya jimbo hilo, ambapo washambuliaji waliviteketeza kwa moto vijiji vya eneo hilo.
Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa kabila la wasio Waarabu la Gimir, mapigano ya kugombea ardhi yalizuka baina ya watu wa kabila la Waarabu na mkulima mmoja wa jamii hiyo ya wasio Waarabu na kusababisha watu wanane wa jamii ya Gimiri kuuawa na vijiji vitatu kuchomwa moto.
Kiongozi wa jamii ya Waarabu ya Riziegat amethibitisha kuwa mapigano yalianza kutokana na mzozo wa kugombea ardhi na kwamba watu wanane wa jamii yao pia wameuawa katika mapigano hayo.
Huko Kordofan Kusini pia mapigano yamezuka baina ya jamii mbili za makundi hasimu ya Waarabu ya Hawazma na Kenana.
Kwa mujibu wa mkazi wa eneo hilo aliyeshiriki kwenye upatanishi, watu wasiopungua 11 wameuawa na wengine 35 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Ameongeza kuwa mapigano yalianza kwa ugomvi baina ya watu wawili na kugeuka kuwa mapambano ya silaha kati ya makundi hayo mawili.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes amesema ametiwa wasiwasi mkubwa na mapigano ya kikabila yaliyozuka katika jimbo la Kordofan Kusini.../