Umoja wa Ulaya waipendelea Uhispania, waionya Algeria
(last modified Sat, 11 Jun 2022 07:25:40 GMT )
Jun 11, 2022 07:25 UTC
  • Umoja wa Ulaya waipendelea Uhispania, waionya Algeria

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Barrell ameonesha waziwazi kuipendelea Uhispania katika mgogoro wake na Algeria kwa kuionya Algiers kuhusu kusimamisha ushirikiano wake na Madrid.

Borrell amesema katika taarifa yake kuwa, uamuzi wa Algeria wa kusimamisha makubaliano yake ya urafiki na ujirani mwema na Uhispania yaliyotiwa saini mwaka 2002, ni jambo lisilokubalika na linatia wasiwasi mkubwa.

Amesema, hivi sasa Umoja wa Ulaya unachunguza madhara ya hatua ya Algeria ya kutotaka tena urafiki na Uhispania hasa katika upande wa mashirika ya fedha na biashara baina ya pande hizo mbili.

Borrell pia amedai kuwa, hatua hiyo ya Algeria ni ya ubaguzi na kwamba Umoja wa Ulaya unajaribu kuwasiliana na Algiers kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Algeria ina mpaka wa baharini na Uhispania

 

Siku ya Jumatano, Ikulu ya Algeria ilitangaza kuwa, imesimamisha ushirikiano wake wa miaka 20 na Uhispania kutokana na nchi hiyo ya Ulaya kuipendelea Morocco katika mgogoro wa Sahara Magharibi.

Umoja wa Ulaya umehamakishwa na hatua ya Algeria ya kutangaza kuwa haitaki tena urafiki na ushirikiano na Uhispania licha ya kwamba Algiers imechukua hatua hiyo baada ya Uhispania kutangulia kuvunja ahadi yake ya ujirani mwema na Algeria.

Umoja wa Ulaya umedai kuwa Algeria inafanya ubaguzi kwenye uamuzi wake huo katika hali ambayo nchi za Ulaya zinaziwekea vikwazo nchi nyingine dunia kwa utashi tu wa Umoja wa Ulaya na bila ya sababu yoyote, isipokuwa tu kutaka kuonesha ubeberu wa madola hayo ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

Tags