Jun 28, 2022 08:01 UTC
  • Zaidi ya 30 wauawa katika mapigano ya kikabila Cameroon

Wanavijiji wasiopungua 30 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuawa katika mapigano ya kikabila huko magharibi ya Cameroon.

Hayo yalisemwa jana Jumatatu na Kasisi Fonki Samuel Forba, msemaji wa Kanisa la Presbyterian nchini Cameroon ambaye ameongeza kuwa, mauaji hayo ya halaiki yalitokea mwishoni mwa wiki katika eneo la Bakinjaw, karibu na mpaka wa Nigeria.

Forba amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, mapigano hayo yalihusisha watu wa makabila ya Oliti na Messaga Ekol, na kwamba zaidi ya watu 30 wameuawa wakiwemo raia watano wa Nigeria, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Asasi za kiraia na duru za kijeshi nchini Cameroon zimethibitisha habari ya kutokea mauaji hayo ya kutisha, zikisisitiza kuwa mgogoro wa kikabila umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu sasa katika eneo la Akwaya.

Maafisa usalama Cameroon

Hivi karibuni, kanali ya Televisheni la al-Jazeera ya Qatar iliripoti kuwa, mapigano ya kikabila yaliyozuka kaskazini mwa Cameroon yamesababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia katika nchi jirani wakihofia usalama wa maisha yao.

Mbali na mapigano hayo ya kikabila, Cameroon inaandamwa pia na hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Tags