Kiongozi wa kijeshi wa Sudan awateua wanajeshi watano kuwa mabalozi
(last modified Mon, 11 Jul 2022 07:48:24 GMT )
Jul 11, 2022 07:48 UTC
  • Kiongozi wa kijeshi wa Sudan awateua wanajeshi watano kuwa mabalozi

Kamanda wa jeshi la Sudan amewateua majenerali watano wa polisi, jeshi na askari usalama kuwa mabalozi wa Khartoum.

Uteuzi huu umejiri sambamba na kuendelea maandamano na ghasia huko Sudan dhidi ya uongozi wa kijeshi. Wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana tokea Oktoba mwaka jana kufuatia mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito ya nchi hiyo. Waandamanaji wanataka wanajeshi waondoke madarakani na wakabidhi madaraka kwa raia, uitishwe uchaguzi wa kidemokrasioa na matatizo ya kiuchumi yapatiwe ufumbuzi. 

Maandamano Sudan dhidi ya uongozi wa kijeshi 

Jenerali Abdel Fattah al Sisi kiongozi mtawala wa kijeshi na ambaye pia ni kamanda wa jeshi la nchi hiyo amewateua majenerali hao watano kama mabalozi wa Khartoum katika Wizara ya Mambo ya Nje. 

Majenerali hao wanatazamiwa kutumwa kuiwakilisha Sudan katika nchi jirani huku Sudan ikiendelea kukumbwa na maandamano dhidi ya serikali ya kijeshi iliyoko madarakani. Jina la Jenerali Jamal Abdulmajid Mkurugenzi wa zamani wa Idara Kuu ya Intelijinsia ambaye ni afisa wa jeshi linaonekana katika orodha hiyo ya mabalozi wateule; na kuna uwezekano akapangiwa kuwa Balozi wa Sudan huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini. 

Aidha Ali Othman Muhammad Yunis ameteuliwa kuwa Balozi kati ya mabalozi hao watano na kuna uwezekano akapangiwa kuiwakilisha Sudan huko Chad.  

Katika upande mwingine, Jenerali Abdel Fattah al Burhan ametoa ujumbe kufuatia kushtadi maandamano huko Sudan na kutoa wito kwa makundi mbalimbali ya kisiasa zikiwemo kamati za mapambano nchini humo kutumia busara na mazungumzo ili kufikia mapatano ya kitaifa. 

Al Burhan ameeleza kuwa, kipindi cha mpito kinaweza kuhitimishwa kwa urahisi huko Sudan na kwamba suala la kufanyika uchaguzi linategemea mazungumzo. Ametoa wito kwa makundi ya kisiasa kuunda vyama ili kujiandaa kwa uchaguzi. 

 

Tags