Miili mingine 133 ya wahajiri yapatika katika pwani ya Libya
Shirika la Hilali Nyekundu limetangaza kuwa miili ya 133 ya wahajiri waliokufa maji hivi karibuni wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya imepatikana katika mji wa Zuwara, magharibi mwa Libya.
Al-Khamis Al-Bosaifi, ofisa wa shirika hilo aliliambia shirika la habari la Reuters jana Jumapili kuwa, aghalabu ya walioangamia katika ajali hiyo ni wanawake na kwamba kuliwepo na miili mitano ya watoto wadogo. Amesema akthari yao wanatoka nchi za chini ya jangwa la Sahara.
Hivi karibuni, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilisema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia. Habari ziliarifu kuwa, aghalabu ya wahajiri waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni raia wa nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri.
Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine 2,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini.