Ivory Coast yaitaka Mali kuwaachilia huru wanajeshi 49 waliokamatwa Bamako
(last modified Thu, 14 Jul 2022 03:17:14 GMT )
Jul 14, 2022 03:17 UTC
  • Ivory Coast yaitaka Mali kuwaachilia huru wanajeshi 49 waliokamatwa Bamako

Ivory Coast imetaka kuachiliwa huru wanajeshi wake 49 waliokamatwa nchini Mali, tukio ambalo huenda likazidisha mvutano kati ya watawala wa kijeshi wa Mali na mataifa mengine ya Magharibi mwa Afrika huku kukiwa na juhudi za kuzima harakati za makundi yenye silaha yenye uhusiano na al-Qaida na Daesh (ISIS) na kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Usalama wa Taifa la Ivory Coast imesema wanajeshi hao, ambao walikamatwa Jumapili iliyopita katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mali katika mji mkuu Bamako, walitumwa nchini humo kama sehemu ya mkataba wa msaada wa usalama na vifaa uliotiwa saini na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali mnamo Julai 2019.

Ivory Coast imetaka wanajeshi hao waachiwe huru mara moja. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi hao wa Ivory Coast walitumwa Mali chini ya mkataba huo, na kwamba waraka unaohusu majukumu yao ulikuwa umetumwa kwa mamlaka ya viwanja vya ndege na serikali ya kijeshi ya Mali kabla ya kuwasili nchini humo.

Hata hivyo serikali ya kijeshi ya Mali imesema wanajeshi hao waliwasili nchini humo bila ruhusa, na kwamba pasipoti za baadhi yao zinaonyesha taaluma zisizo za kijeshi, na kwamba walitoa maelezo tofauti kuhusu majukumu yao. 

Kanali Abdoulaye Maiga msemaji wa serikali ya mpito ya Mali amesema kuwa, ndege mbili zilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mali juzi Jumapili zikiwa na wanajeshi 49, silaha na zana za kivita. 

Amesema, wanajeshi hao walitua Mali kinyume cha sheria na kwamba serikali ya mpito ya nchi hiyo inawatambua kama mamluki na watafikishwa mahakamani kwa tuhuma hiyo.

Serikali ya kijeshi inayotawala Mali tangu Agosti 2020 imekuwa katika msuguano na majirani wa kikanda na duru za kimataifa kwa kushindwa kuandaa uchaguzi huru na kurejesha utawala wa kikatiba.