Mali yamtimua msemaji wa kikosi cha UN nchini humo, MINUSMA
(last modified Thu, 21 Jul 2022 11:01:49 GMT )
Jul 21, 2022 11:01 UTC
  • Mali yamtimua msemaji wa kikosi cha UN nchini humo, MINUSMA

Mali imemfukuza msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MINUSMA), huku uhusiano baina ya Bamako na UN ukizidi kuharibika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali katika taarifa imesema kuwa imempa Olivier Salgado, Msemaji wa MINUSMA saa 72 awe ameondoka nchini humo, kutokana na taarifa isiyokubilika aliyoisambaza hivi karibuni kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kwa kusema, Msemaji huyo wa kikosi cha kulinda amani cha UN pasi na kutoa ushahidi wowote alidai kwenye ujumbe wake wa Twitter kuwa, mamlaka za Mali zilifahamishwa kabla ya kuwasili nchini humo askari 49 wa Ivory Coast.

 Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali imesema nchi hiyo haiwezi kupuuza vitendo vya namna hiyo ambavyo vinadhalilisha ushirikiano na MINUSMA na washirika wengine wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake, Farhan Haq umeleeza kusikitishwa kwake na hatua ya Mali ya kumfukuza nchini humo msemaji wa MINUSMA.

Wanajeshi wa Mali

Mvutano umeongezeka kati ya Mali na Umoja wa Mataifa baada ya mamlaka nchini Mali kuwakamata wanajeshi kutoka Ivory Coast, wakiwemo askari wa kikosi maalumu cha UN, na kuwataja kuwa mamluki.

Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali kupitia barua iliyotumwa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa ilsema kwamba, "kwa sababu za usalama wa taifa, serikali ya Mali imeamua, kuanzia Alhamisi (iliyopita), kusimamisha safari zote za anga za ujumbe huo, ikiwa ni pamoja na zile ambao tayari zimepangwa au kutangazwa."