Lavrov: Russia na Afrika zinataka kupunguza matumizi ya Dola katika biashara zao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i86170-lavrov_russia_na_afrika_zinataka_kupunguza_matumizi_ya_dola_katika_biashara_zao
Russia na washirika wake wa Kiafrika wanajaribu kupunguza hatua kwa hatua utumiaji wa sarafu ya dola ya Marekani na euro katika miamala ya kibiashara ya pande zote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2022 22:41 UTC
  • Lavrov: Russia na Afrika zinataka kupunguza matumizi ya Dola katika biashara zao

Russia na washirika wake wa Kiafrika wanajaribu kupunguza hatua kwa hatua utumiaji wa sarafu ya dola ya Marekani na euro katika miamala ya kibiashara ya pande zote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov amesema mbele ya vyombo vya habari vya Kiafrika kuwa, hali ya sasa ya kijiografia na kisiasa inahitaji marekebisho ya mifumo wa mahusiano baina ya pande mbili.

Amesema, kwanza kabisa, kuna haja ya kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kilojistiki vya kurahisisha biashara baina ya nchi washirika na kurekebisha mfumo wa kifedha ili kuzidhaminia usalama nchi hizo kutokana na uingiliaji wa nchi ajinabi. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, 'tunafanya juu chini kupunguza hatua kwa hatua utumiaji wa sarafu ya dola na euro katika biashara ya pande zote na kwamba Russia inaunga mkono kuanzishwa kwa mfumo huru wa kifedha ambao utazuia athari mbaya zinazoweza kusababishwa na mataifa yasiyo rafiki.

Lavrov ameongeza kuwa, ni muhimu kwa marafiki zetu wa Afrika kuelewa kwamba, Russia itaendelea kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa kuhusu mauzo ya nje ya chakula, mbolea, nishati na bidhaa nyingine muhimu kwa bara la Afrika.   

Sergei Lavrov anatarajia kufanya ziara barani Afrika kuanzia tarehe 24 hadi 28 mwezi huu, ambapo atazitembelea Misri, Ethiopia, Uganda na Jamhuri ya Congo. 

Ushirikiano wa Russia na Afrika 

Ameongeza kuwa, duru za kipropaganda za Magharibi na Ukraine zinafanya kila linalowezekana ili kuiarifisha Russia kama msababishaji wa njaa duniani huku zenyewe zikijivua na suala hilo. 

Amesema, baada ya dunia kukumbwa na janga la corona, nchi za Magharibi zilitumia mfumo wa uchapishaji sarafu kubadili mtiririko wa uuzaji chakula na bidhaa nyingine kwa manufaa yao na hivyo kusababisha hali mbaya kwa nchi nyingine duniani ambazo zinategemea kununua bidhaa muhimu kutoka nje.