Njaa yaua watu 900 katika eneo la Karamoja, Uganda
Mamia ya watu wamepoteza maisha kutokana na makali ya njaa katika eneo la Karamoja, kaskazini mwa Uganda.
Katika kikao na waandishi wa habari mjini Kampala jana Jumatatu, viongozi wa eneo hilo wamesema zaidi ya watu 900 wameaga dunia kutokana na njaa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
Paul Lote, Mwenyekiti wa Kotido, moja ya wilaya za eneo hilo la kaskazini mwa Uganda amesema watu 626 wakiwemo watoto wadogo wa miaka mitatu wamefariki dunia wilayani hapo kutokana na njaa.
Hali kadhalika watu zaidi ya 259 wameaga dunia kwa makali ya njaa katika wilaya ya Kaabong, na wengine karibu 50 katika wilaya ya Napak.

Viongozi wa eneo la Karamoja wamesema msaada wa serikali wa tani 790 za unga wa ugali na maharage umeweza kuwafikia watyu watu 640, kati ya watu 163,000 wa eneo hilo wanaohitaji msaada wa dharura.
Eneo la Karamoja la kaskazini mwa Uganda limekubwa na ukame na baa la njaa kutokana na kutonyesha mvua tokea mwanzoni mwaka huu hadi sasa, jambo lililopelekea kukauka kwa mimea.