Wafanyamapinduzi ya kijeshi wakiri kuwa wameshindwa kuleta mabadiliko Sudan
Naibu Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan amekiri kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa nchini humo yameshindwa kuleta mabadiliko.
Sudan imekuwa ikishuhudia mivutano na machafuko makubwa tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi Oktoba 25, 2021 kwa uongozi wa mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Baada ya mapinduzi hayo, al Burhan aliwaengua madarakani viongozi wa kiraia na tangu wakati huo hadi sasa, Wasudan wamekuwa wakiandamana kila leo kupinga utawala wa kijeshi uliohodhi madaraka ya nchi.
Mgogoro wa hali mbaya ya uchumi na wasiwasi wa kiusalama, navyo pia vimechangia kuongezeka mapigano katika maeneo yaliyoko mbali na mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Shirika la habari la ISNA limeripoti kuwa, Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama Hemeti, Naibu mkuu wa baraza la utawala Sudan amesema: kwa masikitiko ni kwamba hatukuweza kuleta mabadiliko yoyote. Mpango umefeli na hali ya Sudan hivi sasa imekuwa mbaya zaidi.
Hemeti ameongezea kwa kusema: ikiwa kujiondoa vikosi vya majeshi katika ulingo wa siasa kutaifanya Sudan iinuke, sisi tunaliunga mkono hilo."
Kuhusu uwezekano wa yeye mwenyewe kugombea urais, Mohamed Hamdan Dagalo amesema: mimi sina ndoto kubwa za kisiasa, lakini kama nitaona Sudan inasambaratika, nami pia kama mtu mwingine yeyote nitajitosa uwanjani.../