Jeshi la Burkina Faso lakiri kuua raia katika shambulio dhidi ya 'magaidi'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i86584-jeshi_la_burkina_faso_lakiri_kuua_raia_katika_shambulio_dhidi_ya_'magaidi'
Jeshi la Burkina Faso limekiri kuwa liliua raia 'kimakosa' katika operesheni ya kupambana na magenge ya kigaidi kusini mashariki mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2022 21:54 UTC
  • Jeshi la Burkina Faso lakiri kuua raia katika shambulio dhidi ya 'magaidi'

Jeshi la Burkina Faso limekiri kuwa liliua raia 'kimakosa' katika operesheni ya kupambana na magenge ya kigaidi kusini mashariki mwa nchi.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo jana Jumatano imesema kuwa, licha ya kufanikiwa kuua makumi ya magaidi katika mashambulizi ya anga mapema wiki hii baina ya maeneo ya Kompienga na Pognoa mpakani mwa Togo, lakini raia kadhaa waliuawa pia katika operesheni hiyo.

Hata hivyo taarifa hiyo haijaeleza idadi ya raia waliouawa au kujeruhiwa kwenye operesheni hiyo ya kupambana na magenge ya kigaidi kusini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mwezi uliopita, jeshi la Togo pia liliua raia saba kimakosa katika shambulio la anga dhidi ya magaidi, katika eneo hilo hilo ambapo wameuawa raia na wanajeshi wa Burkina Faso. 

Askari wa Burkina Faso

Wanajeshi waliotwaa madaraka Burkina Faso waliahidi kupambana na ugaidi katika nchi hiyo ambayo tangu 2015 imekumbwa na wimbi la ghasia na machafuko yanayohusishwa na harakati za kigaidi zenye mfungamano na makundi ya al-Qaida na Daesh.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, serikali ya Burkina Faso imepoteza udhibiti wa zaidi ya asilimia 40 ya ardhi ya nchi hiyo na mashambulizi ya kigaidi yameongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu.