Waliopanga mapinduzi ya Sudan wakiri, wameshindwa kufikia malengo yao
Mgogoro wa kisiasa na kutoridhika kwa jamii nchini Sudan kumekuwa na taathira kubwa na pana, kwa kadiri kwamba "Mohamed Hamdan Dagalo", anayejulikana kama Hemetti, Makamu wa Rais wa Baraza la Uongozi la Sudan, amekiri kwamba: "Inasikitisha kuwa hatukuweza kufanya mabadiliko yoyote na sasa hali ya Sudan imekuwa mbaya zaidi."
Sudan imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa kisiasa kwa miezi kadhaa kutokana na jeshi kutwaa madaraka ya nchi. Wanajeshi wa Sudan wanaendelea kushikilia madaraka ya nchi hiyo tangu baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir. Wananchi wa Sudan wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara wakitaka kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia hasa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, lakini matakwa hayo hayajatekelezwa hadi sasa.
Kutokana na kushadidi mgogoro wa Sudan katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, taasisi za kieneo na kimataifa na makundi mbalimbali ya kisiasa yameamua kuchukua hatua kwa ajili ya kurejesha amani nchini humo ikiwa ni pamoja na kuitishwa uchaguzi na kukabidhiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia; hata hivyo juhudi hizo hazijazaa matunda.
Nchi hiyo kwa sababu inasumbuliwa pia na mgogoro mkubwa wa kiuchumi sambamba na matatizo ya kisiasa yanayoandamana na machafuko ya kijamii. Wasudani ambao walikuwa na matumaini kwamba kuondolewa madarakani utawala wa miongo kadhaa wa Omar al Bashir kungepelekea kuboreshwa hali ya uchumi ya Sudan sasa wanasumbuliwa na ughali wa maisha, umaskini na ukosefu wa amani na ajira. Kwa sababu hii, wananchi waliowengi wa Sudan wanataka jeshi liondoke madarakani, kukabidhi serikali kwa utawala wa kiraia na kuitishwa uchaguzi wa kidemokrasia. Kwa upande mwingine majenerali wa Sudan bado wanang'ang'ania madarakani na wanatumia mkono wa chuma kukabiliana na wapinzani wao. Vikosi vya usalama na jeshi la polisi la Sudan halistahimili hata maandamano ya amani ya Wasudani, na katika miezi na wiki za hivi karibuni jeshi la Sudan limewashambulia waandamanaji hao kwa mabomu ya machozi, mabomu ya sauti na maji yenye harufu mbaya.
Watawala wa kijeshi wa Sudan wanajaribu kutuliza hali hiyo kwa kutegemea madola ya kigeni, jambo ambalo limewakasirisha zaidi watu wa nchi hiyo. Katika mkondo huo mwaka 2022 watawala hao wa kijeshi wa Sudan walisaini Makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel kwa kufuata maagizo na matakwa ya Marekani. Hata hivyo hatua hiyo haijaifaidisha lolote Sudan katika upande wa masuala ya uchumi kama ilivyokuwa imeahidiwa. Kuhusiana na suala hilo Abdul Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza Tawala la Sudan, alisema wiki kadhaa zilizopita kwamba: "Kuanzishwa uhusiano baina ya Sudan na Israel kulifanyika kwa takwa la Marekani, na Washington ilitangaza kuwa suala hilo ndiyo sharti la kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Sudan."
Kwa sasa hali ya Sudan inaripotiwa kuwa mbaya sana na waandamanaji wanaopinga utawala wa kijeshi wametangaza kuwa, wataendeleza maandamano hayo hadi kutakapoundwa serikali ya kiraia.
Kutokana na hali hiyo, Volker Peretz, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hali mbaya inayotishia sekta ya siasa, jamii na uchumi wa Sudan na kuisema: "Wakati wa watu wa Sudan kufikia suluhu na mapatano ya kisiasa ili kujiondoa katika mgogoro wa sasa ni mdogo, na mazungumzo yatakayofanyika katika anga ya utulivu pekee ndiyo yanayoweza kuwa na matokeo mazuri na ya kuridhisha."