Wasudan waandamana kuunga mkono mpango wa kisiasa wa Jenerali al-Burhan
Duru za habari zimeripoti kuwa, mamia ya Wasudan wameandamana kuunga mkono mpango wa kisiasa uliobuniwa na mkuu wa majeshi Brigedia Jenerali Abdel Fattah el-Burhan kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Katika miezi ya karibuni, Sudan imekumbwa na maandamano yaliyotawaliwa na fujo na machafuko makubwa kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa Oktoba 25, 2021 dhidi ya serikali ya kiraia iliyokuwa ikiongozwa na waziri mkuu Abdallah Hamdok.
Waandamanaji hao wamekuwa wakitaka jeshi liachie madaraka na kujiondoa kwenye ulingo wa siasa kwa kukabidhi hatamu za uongozi kwa viongozi wa kiraia, uitishwe uchaguzi wa kidemokrasia na kutatuliwa matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi hyo.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mamia ya watu wameandamana katika mji mkuu Khartoum kuunga mkono mpango wa kisiasa uliobuniwa na kupndekezwa na kamanda wa majeshi Jenerali al Burhan, ambaye ametaka kuwepo na mwafaka wa kitaifa na kueleza matumaini yao kwamba mpango huo utahitimisha mgogoro wa nchi hiyo.
Kongamano chini ya anuani Ubunifu wa Kisiasa wa Kuinasua Sudan na Mgogoro wa Kisiasa ulifanyika siku ya Jumamosi katika mji mkuu Khartoum na kuhudhuriwa na wawakilishi wa baadhi ya vyama vya siasa. Washiriki wa kongamano hilo walisisitizia umoja baina ya Wasudan wote.
Hata hivyo makundi na mirengo mikuu ya wapinzani wa serikali ya kijeshi inayoshikilia madaraka ya nchi hawakushiriki katika kongamano hilo.
Alipohutubia kongamano la Jumamosi, Naibu Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama Hemeti, alisema, jeshi limeamua kutoa fursa kwa makundi ya kisiasa ya kitaifa yafanye mazungumzo na kufikia mwafaka bila ya uingiliaji wa wanajeshi.../