Juhudi za kuiondoa Sudan kwenye mkwamo wa kisiasa
(last modified Tue, 16 Aug 2022 04:08:41 GMT )
Aug 16, 2022 04:08 UTC
  • Juhudi za kuiondoa Sudan kwenye mkwamo wa kisiasa

Juhudi za kutatua mzozo wa kisiasa nchini Sudan zinaendelea. Kuhusiana na hilo, Abd al-Fattah Al-Burhan, mtawala wa kijeshi wa Sudan, ametoa wito wa "kufikiwa makubaliano ya kitaifa" ili kuondokana na mgogoro wa sasa wa kisiasa nchini humo.

Huku vyama vingi vikipinga wito wake huo, baadhi ya wananchi ambao hawajaridhishwa na mivutano ya kisiasa nchini, wamefanya maandamano wakiunga mkono mpango wa "Al Burhan" wa kumaliza mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.

Wasudan wanatumai kwamba kwa kuondolewa jeshi kutoka madarakani, njia ya kutatua mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo itafunguliwa. Abdul Fattah al-Barhan, mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan, alisema katika hotuba yake katika Siku ya Jeshi kwamba: "Jeshi litatatekeleza  matarajio halali ya watu wa Sudan ya kufikia mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia katika kivuli cha serikali moja."

Al-Barhan ametoa kauli hiyo huku mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ambao umeendelea kwa muda mrefu ukifanya hali kuwa ngumu zaidi kwa watu wa nchi hiyo. Hivi sasa Sudan inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi na machafuko ya kijamii yanaendelea katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.

Wasudan, ambao walitarajia kwamba hali ya kiuchumi ingeboreka baada ya kupinduliwa rais wa miaka 30 Omar al-Bashir, sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya ughali wa maisha, umaskini na ukosefu wa usalama na ajira.

Farhan Haq", Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, amesema kuhusiana na suala hilo: "Hivi sasa, zaidi ya watu milioni 14 nchini Sudan wanahitaji msaada."

Katika hali hiyo, wananchi walio wengi wa Sudan wanataka jeshi liondoke madarakani na kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia.

Ingawa jeshi limeahidi kuondoka madarakani na kufanya uchaguzi huru nchini Sudan, lakini vyama vikuu vya kisiasa vinaamini huo ni uongo mkubwa na wala havina imani hata kidogo na ahadi zinazotolewa na watawala wa kijeshi. Hali ya kutoaminiana ni kubwa kiasi kwamba vyama vikuu viwili vya upinzani havikushiriki mazungumzo ya hivi karibuni.

Wapinzani wanaamini kuwa jeshi halitaondoka madarakani kwa sababu linataka kuainisha sera za kigeni za nchi hiyo na kudhibiti benki kuu ya Sudan ili kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika uchumi wa nchi.

Kwa mtazamo wa wapinzani, katika hali hiyo, uundaji wa serikali ya kiraia hautakuwa na maana kwa sababu serikali kama hiyo itakuwa chini ya udhibiti wa wanajeshi.

Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi Sudan

Pamoja na hayo waungaji mkono wa utawala wa Jenerali Burhan wanansema maandalizi ya jeshi kuondoka kwenye uwanja wa kisiasa yametoa fursa nzuri kwa Sudan kujiondoa katika mzozo wa kisiasa. Baadhi ya raia wanauchukulia mpango wa makubaliano ya kitaifa na jeshi kuafiki kufanya uchaguzi wa kidemokrasia kuwa fursa ambayo inapaswa kutumika kurejesha utulivu wa kisiasa nchini.

Pamoja na hayo Wasudan wameonyesha kwa mara nyingine tena kwamba wamechoshwa na hali ya sasa na wanataka kuendelezwa juhudi za mazungumzo ili kujiondoa katika hali hiyo.

Ni kwa msingi huo ndio mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi hasimu yanatazamiwa kuendelea ili kutafuta suluhu ya kujiondoa katika hali iliyopo.

Mani Manawi, mkuu wa kamati ya mawasiliano ya kisiasa ya Kundi la Makubaliano ya Kitaifa, anasema: Makundi ya Sudan yamekubaliana juu ya rasimu ya kisiasa kuhusu katiba ya kipindi cha mpito, vigezo vya kuchagua waziri mkuu wa serikali ya kiraia, na majukumu ya serikali ya mpito.

Ingawaje kutokana na mgawanyiko wa kisiasa na hitilafu za kimtazamo baina ya vyama vya Sudan, mzozo wa kisiasa wa Sudan hauonekani kutatuliwa mara moja, lakini matukio ya hivi sasa yanaonyesha kuwa Sudan haina budi ila kujaribu kufikia makubaliano ya kisiasa.

 

Tags