Chama tawala kinaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi Angola
(last modified Thu, 25 Aug 2022 10:46:37 GMT )
Aug 25, 2022 10:46 UTC
  • Chama tawala kinaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi Angola

Matokeo ya awali katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Angola hapo jana yanaonesha kuwa chama tawala cha MPLA kinaongoza.

Kwa mujibu wa matokeo ya asilimia 33 ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE), chama tawala cha People’s Movement for the Liberation of Angola (MPLA) kinaongoza kwa asilimia 60 ya kura.

Katita taarifa leo Alkhamisi, CNE imesema chama kikuu cha upinzani cha National Union for the Total Independence of Angola (UNITA) kimeambulia asilimia 33.85 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.

Hata hivyo chama hicho cha upinzani kinachoongozwa na Adalberto Costa Junior, kinasisitiza kuwa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE) si ya kutegemewa na hayana itibari.

Abel Chivukuvuku, mgombea mwenza wa urais wa chama cha UNITA amesema hawayatambuia matokeo yaliyotangazwa, na kwamba watatangaza matokeo yao wenyewe, kwa kuzingatia data sawa na zilizotumiwa na Tume ya Uchaguzi.

Rais wa Angola (kushoto) na mgombea wa upinzani

Uchaguzi huo umetajwa kuwa na ushindani wa aina yake na mkali kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa vuguvugu la siasa za vyama vingi mwaka 1992 nchini Angola.

Chama tawala cha MPLA kimetawala Angola tangu nchi hiyo ijipatie uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975. Rais aliyeko madarakani João Lourenço,  anayewania muhula wa pili anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha upinzani cha UNITA Adalberto Costa Junior.