Zanzibar: Tuna hamu ya kupanua uhusiano wetu na Iran
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar amesema anatumai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaimarisha na kupanua uhusiano wao wa pande mbili.
Nasser Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya wa Zanzibar amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian visiwani humo.
Waziri Mazrui alisema hayo baada ya kumpokea Amir-Abdollahian na ujumbe aliofuatana nao akiendelea na safari yake nchini Tanzania. Amesema Wazanzibari na Wairani wanaweza kuwa na uhusiano mzuri zaidi, kwani ni mandugu wenye utamaduni unaofanana.
Amir-Abdollahian aliwasili katika uwanja wa ndege wa Zanzibar Jumatano jioni, na kukaribishwa na Nasser Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya wa Zanzibar na viongozi wengine wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dakta Hussein Mwinyi na kujadili mahusiano kati ya nchi ya Iran na Zanzibar.
Akiwa jijini Dar es Salaam hapo jana, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeko ziarani nchini Tanzania katika ziara ya kulitembelea bara Afrika akitokea Mali alisema kuwa, Afrika ni moja ya vipaumbele vikuu vya diplomasia ya kiuchumi ya Iran.
Sambamba na kuashiria uwezo wa kiuchumi, kiviwanda na teklojia wa Iran alisisitiza kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni kuhusu kustawisha uhusiano wa kiuchumi na mataifa ya Kiafrika hususan Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.