Abdul-Fattah al-Burhan afanya mabadiliko makubwa katika jeshi la Sudan
Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, kiongozi wa kijeshi nchini Sudan, ametangaza mabadiliko makubwa ya uongozi katika jeshi la nchi hiyo, huku msukosuko wa kisiasa na kiuchumi ukiendelea kushuhudiwa nchini humo.
Duru za karibu na jeshi la Sudan zinaripoti kuwa, mabadiliko hayo yanajumuisha kubadilishwa makanda wakuu wa vikosi vya jeshi la nchi kavu, kamandi ya operesheni, kikosi cha uokozi na Mkaguzi Mkuu wa jeshi.
Siku chache zilizopita pia, kiongozi huyo wa kijeshi wa Sudan anayekabiliwa na upinzani mkali wa wananchi ambao wamekuwa wakiandamana mtawalia kupinga uongozi wake alitangaza kufanya mabadiliko katika kikosi cha anga.
Wachambuzi wa mambo wameyataja mabadiliko hayo katika vikosi vya jeshi kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka jana yaliyouondoa madarakani utawala wa kiraia.
Baadhi ya weledi wa masuala ya kisiasa ya Sudan wanaamini kuwa, hatua hiyo ya jenerali Abdul-Fattah al-Burhan inatokana na hofu aliyonayo ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi dhidi yake wakati huu ambapo Sudan inakabiliwa na sokomoko la kiuchumi na kisiasa.
Sudan ilietumbukia kwenye lindi la machafuko na mapigano kati ya jeshi na raia wanaopinga utawala wa kijeshi, tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi Oktoba 25, 2021. Licha ya wanajeshi kuahidi kwamba watakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini wananchi wanaopinga nchi hiyo kutawaliwa na jeshi wanataka majenerali wa jeshi wang'atuke madarakani na nchi hiyo kuongozwa katika kipindi cha mpito na utawala wa kiraia kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia.
Sudan, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imekuwa ikiyumba kutokana na uchumi unaoporomoka kutokana na miongo kadhaa ya kutengwa kimataifa na usimamizi mbovu chini ya kiongozi wa zamani wa Omar al-Bashir.