Viongozi wa upinzani Sudan wasisitiza kuunga mkono maandamano ya wananchi
Viongozi wa harakati na makundi ya uhuru na mageuzi nchini Sudan wamesisitiza kuwa, wanaunga mkono maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo kwa ajili ya kuuangusha utawala wa kijeshi unaoongozwa na jenerali Abdul-Fattah al-Burhan.
Taarifa ya viongozi hao imeeleza kwamba, watawala wa kijeshi wamekata tamaa katika kukwamisha maandamno ya wananchi yanayowapinga na ndio maana wameamua kuwarejesha katika nyadhifa maelfu ya watu wenye mfungamano na utawala wa zamani.
Jeshi la Sudan, likiongozwa na Burhan, lilinyakua madaraka Oktoba mwaka jana, baada ya kumzuilia Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na viongozi wengine wa kiraia na kuvunja serikali ya mpito ya mwaka mmoja pamoja na baraza tawala la kijeshi na kiraia lililoundwa baada ya kuondolewa madarakani Rais wa muda mrefu wa Omar al-Bashir.
Hatua hiyo iliibua hasira na hasira katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika na kuibua malalamiko ya kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Nchi hiyo imekumbwa na maandamano tangu wakati huo ambayo yamesababisha vifo vya watu mia moja na mamia kujeruhiwa.
Sudan ilietumbukia kwenye lindi la machafuko na mapigano kati ya jeshi na raia wanaopinga utawala wa kijeshi, tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi Oktoba 25, 2021. Licha ya wanajeshi kuahidi kwamba watakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini wananchi wanaopinga nchi hiyo kutawaliwa na jeshi wanataka majenerali wa jeshi wang'atuke madarakani na nchi hiyo kuongozwa katika kipindi cha mpito na utawala wa kiraia kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia.
Sudan, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imekuwa ikiyumba kutokana na uchumi unaoporomoka kutokana na miongo kadhaa ya kutengwa kimataifa na usimamizi mbovu chini ya kiongozi wa zamani w nchi hiyo Omar al-Bashir.