Umoja wa Mataifa wataka viongozi wa Eritrea wapelekwe ICC
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuwekewa vikwazo na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC viongozi na wanasiasa wa Eritrea, kwa tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu.
Wachunguzi wa maswala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanawatuhumu viongozi wa Eritrea kuwa wamekanyaga haki za binadamu na kuhusika katika jinai mbali mbali za kutisha kama mauaji, ukandamizaji na ubakaji; huku wakilitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuwawekea vikwazo viongozi na kuwasilisha mafaili yao mbele ya mahakama ya ICC huko mjini Hague, Uholanzi. Ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, jina hizo dhidi ya binadamu zimekuwa zikifanywa na viongozi na wanasiasa wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika tangu ijipatie uhuru mwaka 1991.
Ripoti hiyo imefichua kuwa, mbali na mauaji, ubakaji na ukandamizaji, watawala wa nchi hiyo changa ya Kiafrika wamekuwa wakifanya biashara ya utumwa mbali na kuwalazimisha vijana kutumika jeshini kwa muda usiojulikana.
Baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na jinai hizo ni maafisa wa ngazi za juu serikalini na haswa wanaotoka chama tawala cha People’s Front for Democracy and Justice na makamanda waandamizi wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.