Mafuriko yaliyosababishwa na mvua yaua watu zaidi ya 130 nchini Sudan
Watu 134 wamepoteza maisha nchini Sudan baada ya kusombwa na maji kufuatia mafuriko makubwa yanayosababishwa na mvua kali inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Baraza la kijeshi linalotawala Sudan limesema mbali na watu hao kupoteza maisha, wengine 120 wamejeruhiwa lakini pia makaazi ya watu yameharibiwa, ikiwemo mimea ya wakulima mashambani.
Nyumba ambazo zimeharibiwa na mafuruko, zinakadiriwa kuwa zaidi ya 128,000 na tayari serikali imetangaza hali ya dharura katika majimbo 18 ya nchi hiyo.
Ongezeko la vifo limeripotiwa, kutoka watu 112 mapema mwezi huu hadi 134, huku jimbo la Kordofan Kaskazini likiongoza kwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo.
Majimbo mengine yaliyoathiriwa na mafuriko hayo ni pamoja na Gedaref, Kassala na Darfur ambalo kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, limeathiriwa zaidi.
Umoja wa Mataifa unahofia kuwa, kufikia mwisho wa mwaka huu huenda watu 460,000 wakaathiriwa na mafuriko hayo nchini Sudan.../