Oct 21, 2022 04:13 UTC
  • Afrika CDC: Mripuko wa Ebola Uganda unaweza kudhibitiwa

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimesema kuna hatari ya mripuko wa Ebola unaoshuhudiwa nchini Uganda kusambaa katika nchi nyingine, lakini msambao huo unaweza kudhibitiwa hivi sasa.

Ahmed Ogwell, Kaimu Mkurugenzi wa Afrika CDC alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao na kuongeza kuwa, "Hatari ingalipo, lakini (mripuko wa Ebola) unaweza kudhibitiwa."

Amesisitiza kuwa, katika mazingira ya sasa, hakuna ulazima wa kuchukua hatua kamili za kuweka vizuizi na sheria kali za kudhibiti msambao wa virusi hivyo.

Ogwell amesema kuna mpango wa kuzindua chanjo za majaribio za Ebola, ingawaje hajaeleza siku ya kufanya uzinduzi huo au ni lini wataanza kuzifanyia majaribio chanjo hizo za kukabiliana na maradhi hayo hatarishi.

Tayari serikali ya Uganda imetangaza karantini na kuzuia kutoka na kuingia katika miji ya Mubende na Kasanda kwa muda wa siku 21 ili kuzuia kuenea kwa maradhi hayo. 

Mripuko wa Ebola Uganda

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi sasa kesi 60 za maradhi hayo zimethibitishwa kutokea nchini Uganda, kesi 20 zinashukiwa kuwa za maradhi hayo, huku watu 44 wakiaga dunia kwa maradhi hayo tokea mripuko wa sasa uripotiwe mwezi uliopita.

Hata hivyo Wizara ya Afya ya Uganda imetangaza baada ya kuthibitisha vifo vya watu 5 hivi karibuni kwamba, hadi sasa watu 254 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo.  

Tags