Oct 24, 2022 04:02 UTC
  • Hujuma za magaidi zaongezeka kwa 300% Afrika licha ya operesheni za US

Ripoti mpya ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inaonesha kuwa, mashambulizi ya magenge ya wanamgambo yameongezeka kwa asilimia 300 katika nchi za Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Kituo cha Mafunzo ya Kistratajia ya Afrika cha Pentagon kimesema katika ripoti mpya ya mwezi Septemba kwamba, magharibi mwa eneo la Sahel na Somalia ndiyo maeneo yaliyoshuhudia ongezeko la hujuma za kigaidi.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, asilimia 95 ya mashambulio ya kigaidi katika maeneo hayo ya Afrika yalifanywa na magenge yenye mfungamano na Daesh (ISIS) na al-Qaeda kama vile al-Shabaab.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani ni kuwa, matukio 2,221 ya umwagaji damu katika kipindi kilichotajwa, yanaashiria ongezeko la asilimia 45 ndani ya wastani wa miaka mitatu, baina ya 2018-2020.

Ripoti hiyo ya Pentagon imetolewa wakati huu ambapo Marekani kwa muda sasa inaendeleza operesheni za kijeshi katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

Wanajeshi vamizi wa US

Hii ni katika hali ambayo, maelfu ya Waethiopia walifanya maandamano ya nchi nzima siku ya Jumamosi kulaani kile walichokitaja kama uingiliaji wa madola ya kigeni, hasa Marekani, katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Waandamanaji hao walisema nchi za kigeni zinapaswa kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Ethiopia na zinapaswa kuacha kuunga mkono vikosi vya waasi, haswa kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) na washirika wake

Tags