Watu 230 wauawa, 200 wajeruhiwa katika mapigano ya kikabila Sudan
Waziri wa Afya wa Sudan amesema watu wasiopungua 230 wameuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vijiji kadhaa vya jimbo la Blue Nile, kusini magharibi mwa nchi.
Gamal Nasser al-Sayed amesema hayo katika mahojiano na gazeti la the Gurdian na kuongeza kuwa, zaidi ya watu 30,000 wamekimbia makazi yao katika vijiji vinane vya eneo la Wad al-Mahi katika jimbo hilo la Blue Nile kufuatia mapigano hayo ya kikabila.
Waziri wa Afya wa Sudan ameongeza kuwa, wanawake na watoto wadogo katika jimbo hilo wanasumbuliwa na malaria, katika hali ambayo idara ya afya haina fedha za kutosha za kuwasaidia.
Mapigano katika eneo lenye matatizo la Blue Nile nchini Sudan yalizuka wiki iliyopita baada ya kuripotiwa mzozo wa ardhi kati ya watu wa kabila la Hausa na makundi hasimu.
Ripoti zinaeleza kuwa, mapigano hayo yamejikita zaidi katika eneo la Wadi al-Mahi yapata kilomita 500 kusini mwa mji mkuu Khartoum. Tayari viongozi wa Sudan wametangaza hali ya hatari baada ya kutokea mauaji ya hayo kkatika jimbo la Blue Nile.
Mapigano haya ya hivi sasa ni wimbi jipya la ghasia za kikabila ambazo zimeenea kote nchini Sudan licha ya kutiwa saini mkataba wa amani wa nchi nzima miaka miwili iliyopita.