Oct 27, 2022 13:00 UTC
  • Afrika CDC: Mlipuko wa Ebola nchini Uganda

Shirika la juu zaidi la afya ya umma barani Afrika (Afrika CDC) limetangaza leo Alhamisi kwamba mlipuko wa Ebola nchini Uganda bado unadhibitiwa, licha ya kuongezeka kwa kesi za maambukizi ya ugonjwa huo hadi katika mji mkuu, Kampala.

Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), amesema kwamba, mlipuko wa Ebola nchini Uganda bado unadhibitika, na kuongeza kuwa, kwa sasa haiwezekani kutoa makadirio yoyote ya jinsi ya kuenea kwa ugonjwa huo katika siku za usoni."

Virusi vinavyoenea nchini Uganda ni aina ya Ebola ya Sudan, ambayo hakujapatikana chanjo iliyothibitishwa ya kukabiliana navyo, tofauti na aina ya kawaida ya Zaire iliyoonekana wakati wa milipuko ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakati huo huo Serikali ya Uganda imetangaza kuwa imezidisha vituo vya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ulioiathiri nchi hiyo ya Mashariki mwa Afrika huku idadi ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo ikiongezeka na kufikia 30.

Watu wengine 109 wameambukizwa virusi hivyo katika mlipuko wa sasa wa Ebola nchini Ugada.

Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth, amesema serikali ya Kampala imezidisha vituo vya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Katika upande mwingine maafisa wa mji mkuu Kampala wamesema kuwa watoto sita wa familia moja ya mji huo wamepata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

Watoto hao sita ndugu wa familia moja walipata maambukizi baada ya ndugu yao aliyetoka katika moja ya wilaya zilizoathiriwa zaidi kwenda kuishi nao, na baadaye kufariki dunia.

Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth Aceng anasema ana wasiwasi mkubwa kuhusu kusambaa kwa virusi vya Ebola katika maeneo ya mijini, ambayo yana idadi kubwa ya watu.

Tags