Wanafunzi wa vyuo vikuu Sudan wataka walioanzisha mapigano Blue Nile wahukumiwe
(last modified Sun, 30 Oct 2022 03:04:47 GMT )
Oct 30, 2022 03:04 UTC
  • Wanafunzi wa vyuo vikuu Sudan wataka walioanzisha mapigano Blue Nile wahukumiwe

Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu katika jimbo la Blue Nile nchini Sudan imefanya mgomo katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu mjini Khartoum ikitaka kusitishwa mapigano katika jimbo hilo.

Ni baada ya Waziri wa Afya wa Sudan kutangaza kuwa watu wasiopungua 230 wameuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vijiji kadhaa vya jimbo la Blue Nile, kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Wanafunzi waliofanya mgomo katika vyuo vikuu vya Khartoum wametoa wito wa kufunguliwa mashtaka wahusika wa mapigano na mauaji ya raia katika jimbo la Blue Nile.  

Wanafunzi hao pia wameyataka mashirika ya kimataifa kushughulikia hali ya kibinadamu katika eneo la Blue Nile baada ya kuanza mapigano ya kikabila ambayo yamesababisha mauaji mamia ya raia.

Vilevile wametoa wito wa kusitishwa mapigano hayo na kurejeshwa utawala wa sheria katika jimbo hilo. 

Wanafunzi hao wa vyuo vya Sudan pia wameitaka Serikali ya kijeshii ya nchi hiyo kuchukue jukumu la kusitisha vita katika eneo la Blue Nile na kuilaumu serikali hiyo kwamba imeshindwa kukomesha migogoro ya kikabila ya Sudan hususan katika eneo la Blue Nile. 

Sudan

Mapigano katika eneo lenye matatizo la Blue Nile nchini Sudan yalizuka wiki iliyopita baada ya kuripotiwa mzozo wa ardhi kati ya watu wa kabila la Hausa na makundi hasimu.

Ripoti zinaeleza kuwa, mapigano hayo yamejikita zaidi katika eneo la Wadi al-Mahi yapata kilomita 500 kusini mwa mji mkuu Khartoum.  Tayari viongozi wa Sudan wametangaza hali ya hatari baada ya kutokea mauaji ya hayo katika jimbo la Blue Nile.

Tags