Rais wa Kenya atangaza vita dhidi ya waasi wa M23 wa DRC
(last modified Thu, 03 Nov 2022 02:30:47 GMT )
Nov 03, 2022 02:30 UTC
  • Rais wa Kenya atangaza vita dhidi ya waasi wa M23 wa DRC

Rais William Ruto wa Kenya ametangaza habari ya kutumwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kwenda kukabiliana na magenge ya wanamgambo likiwemo kundi la waasi la M23.

Rais Ruto alitangaza hayo jana Jumatano jijini Nairobi katika hafla ya kuwaaga wanajeshi hao wa Kenya, ambao anasisitiza kuwa wanaenda DRC katika operesheni ya kulinda utu.

Dakta Ruto amesema, "Kama majirani, mustakabali wa DRC unafungamana na mustakabali wetu. Hatutaruhusu kundi lolote la wanamgambo, waasi, majambazi na magaidi kukwamisha mafanikio yetu yenye mfungamano."

Aprili mwaka huu, viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) waliafikiana juu ya kuunda kikosi cha pamoja cha kusaidia kurejesha usalama katika eneo hilo la Afrika. Kenya itaongoza kikosi hicho cha kieneo ambacho kina wanajeshi pia wa Burundi, Uganda na Sudan Kusini.

Agosti mwaka huu, Kenya ilipeleka zaidi ya wanajeshi wake 200 kushiriki katika operesheni za kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo chini ya mwavuli wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa maarufu kwa jina la MONUSCO.

Kwa miaka kadhaa sasa, serikali ya Kenya imekuwa na siasa za kupeleka wanajeshi wake kushiriki kwenye operesheni mbalimbali za kulinda amani.

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF)

Kenya imetuma wanajeshi DRC katika hali ambayo, wakazi wa mji wa Goma mashariki mwa DRC usiku wa kuamkia jana Jumatano walifanya maandamano na kuteketeza kwa moto magari ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, wakisisitiza kuwa ujumbe wa MONUSCO unapaswa kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, kwani uwepo wake haujasaidia chochote katika kurejesha usalama na uthabiti nchini humo.

Wananchi wa Kongo DR wanakisisitiza kuwa, kikosi hicho cha UN kimeshindwa kukabiliana na harakati na mashambulizi ya kundi la waasi la M23.

 

Tags