Serikali ya Kenya yaainisha muda wa kuondoka wakimbizi katika kambi ya Daadab
Serikali ya Kenya imeainisha muhula wa kuondoka maelfu ya wakimbizi wanaoishi kwenye kambi ya Dadaab nchini humo.
Serikali ya Kenya imepanga kuwaondoa na kuwarejesha makwao wakimbizi laki tatu kutoka katika kambi kubwa zaidi ya kuwahifadhi wakimbizi duniani ya Dadaab inayopatikana nchini Kenya ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Kambi ya Dadaab iko umbali wa kilomita 100 kutoka mpaka wa pamoja wa Kenya na Somalia, huku ikitambulika kama kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani kwa kutoa makazi kwa raia karibu laki tano.
Kambi hiyo iliasisiwa mwaka 1991 baada ya kuanguka utawala wa dikteta Mohammed Siad Barre wa Somalia na kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe na mchafuko katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Ukame, baa la njaa la muda mrefu wa vita vya ndani katika nchi za eneo, vilisabaisha kambi ya Dadaab taratibu kubadilika na kuwa mji na hivi sasa pia baada ya kupita miaka 25, kambi hiyo inawahifadhi wakimbizi wengi ambao ni raia kutoka Somalia na nchi nyinginezo kadhaa. Serikali ya Kenya kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka jana ilisisitiza kuwa kambi ya Dadaab itafungwa baada ya kutokea shambulio la magaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa. Kuwepo wasiwasi wa kukaririwa mashambulizi ya kigaidi ya kundi la al Shabab ambalo lilikiri kuhusika na shambulio hilo huko Garissa, kulizidisha hofu kwa viongozi wa Kenya ya kuwepo uwezekano wa kujipenyeza nchini humo kundi hilo la kigaidi.
Wakati huo viongozi wa Kenya walilitaka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) kuwaondoa wakimbizi wa Kisomali wanaoishi katika kambi ya Dadaab katika muda wa miezi mitatu.
Muhula huo ulioainishwa na serikali ya Kenya hata hivyo ulimalizika bila hata Umoja wa Mataifa kuchukua hatua yoyote katika uwanja huo. Hii ni katika hali ambayo mwezi Novemba mwaka 2013 maafikiano ya pande tatu yalifikiwa kati ya Kenya, Somalia na UNHCR; ambapo kwa mujibu wake mazingira yalipaswa kuandaliwa kwa ajili ya kuwarejesha makwao kwa hiari wakimbizi wa Kisomali kutoka kwenye kambi hiyo. Serikali ya Kenya iliwafahamisha maafisa husika wa Umoja wa Mataifa kuwa nchi hiyo haiwezi tena kuwa mwenyeji wa idadi hiyo kubwa ya wakimbizi. Hatua ya kushambuliwa kituo cha biashara cha West Gate jijini Nairobi mwezi Septemba mwaka 2013 iliwachochochea pia viongozi wa Kenya kuchukua uamuzi wa kuifunga kambi ya Dadaab na kuwarejesha nchini kwao wakimbizi wa Kisomali. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya pande tatu, hadi kufikia mwezi Februari mwaka juzi wakimbizi karibu laki moja walikuwa tayari wamerejeshwa katika miji ya Baidoa na Kismayu kusini mwa Somalia.
Upuuzaji wa Umoja wa Mataifa katika kutoa radiamali yake kwa serikali ya Kenya ulipelekea tarehe 6 mwezi Mei mwaka huu serikali ya Kenya kutishia kwa mara nyingine kuzifunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma. Wizara ya Ulinzi ya Kenya imesisitiza kuwa kambi za wakimbizi nchini humo zinapasa kufungwa ili kudhamini maslahi ya taifa. Viongozi wa Kenya wanaamini kuwa kambi za Dadaab na Kakuma zimegeuzwa na kuwa vituo vya kusajili wanamgambo wapya kwa ajili ya kundi la al Shabab huko Somalia. Hasa ikizingatiwa kuwa gharama za kuendesha kambi hizo zimekuwa zikizidisha mzigo kwa uchumi wa Kenya.
Weledi wa mambo kwa upande wao wanaamini kuwa, kukosekana fursa za kazi na kushindwa kujidhaminia mahitaji ya chakulaa na makazi salama, yote hayo yameyafanya mazingira ya kurejea wakimbizi katika maisha ya kawaida kuwa magumu. Baadhi ya wakimbizi watarudi katika maeneo yanayoshikiliwa na al Shabab kwa kuzingatia muundo wa kikabila wa huko Somalia. Mchakato huo unamaanisha kuwa baada ya kuondoka wakimbizi huko Dadaab na Kakuma, serikali ya Kenya na Umoja wa Mataifa hautawasimamia na kuwadhibiti wakimbizi hao, na watakuwa huru kwenda popote wanapotaka.